Tangazo la Shiwata created by innowise(Banners)



Saturday, January 18, 2014

SHIWATA yakabidhi vyeti 1,000 kwa wasanii

Na Peter Mwenda

 MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umetoa vyeti kwa wasanii 1,000 waliofanya kazi zao vizuri katika kipindi cha mwaka 2013-2014 katika kongamano lililofanyika ukumbi wa Lamada, Ilala Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na wasanii,wanamichezo,wanahabari na vijana zaidi ya 1,500 mgeni rasmi Rais Jakaya Kikwete aliyewakilishwa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana utamaduni na Michezo, Amos Makala aliwaasa wasanii watumie kipato chao kujiandaa kwa maisha ya baadaye baadaye.

Makala aliwataka wasanii kujiunga na Shiwata na kujenga nyumba zao za pamoja kwa gharama nafuu katika kijiji cha Mwanzega, Mkuranga ambako mpaka sasa zimejenga nyumba 55 kati ya hizo 38 zimekabidhiwa wenyewe na nyingine zinaendelea kujengwa ambazo zitakabidhiwa wenyewe Machi mwaka huu.

Katika risala ya Shiwata kwa mgeni rasmi iliyosomwa na Kanali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Juma Ikangaa ambaye pia aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Tanzania (TAA),SHIWATA imetoa ekari 5 kwa ajili ya Rais Kikwete ajenge  nyumba katika kijiji cha Mwanzega Mkuranga na ekari 5 nyinguine kwaq ajili ya kilimo katika kijiji cha Ngarambe, Mkuranga.

Pia risala hiyo imemuomba Rais Kikwete asaidie kurudisha vituo vya burudani, viwanja vya michezo, na wapewe sehemu ya bustani ya mnazi Mmoja kwa ajili ya maonesho ya wazi, ujenzi wa makao makuu ya Mtandao na ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kazi zao.

Pia SHIWATA iliomba kuwepo mwakilishi wa wasanii katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na taasisi zote za Umma kama Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Sheria yHaki Miliki iangaliwe upya kwani ina upungufu.

Katika kongamano hilo SHIWATA imezindua Mpango wake wa umoja ambao utawasaidia wasanii kujitegemea wenyewe katika kazi mbalimbali badala ya kusubiri misaada kutoka kwa wafadhili kwa kutoa misaada kwa wasanii wachanga kurekoodi miziki yao,kurekodi filamu, na kupata michezo.

Taarifa ya SHIWATA iliyotolewa na Mwenyekiti wake, Cassim Taalib alisema mpango huo utawafaidisha wasanii  kupata fedha za matibabu, mazishi pamoja na kununua na kusambaza kazi za wasanii.

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga mstaafu, Henry Clemence aliyetoa mada kuhusu maadili mema na juzalendo, aliwataka wasanii kuwa na tabia nzuri wanapokuwa ndani na nje ya nchi kwa mavazi ya heshima na mwenendo bora.

Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa alisema athari za matumizi ya dawa za kulevya zinaiaibisha Tanzania inayofahamika kuwa kisima cha wananchi waadilifu kwa wanavyotumiwa wasanii na wanamichezo kusaifirisha na kutumia dawa za kulevya.

Mgeni rasmi Naibu Waziri Makala aliyemwakilisha Rais Kikwete aliwaasa wanamichezo kutumia fedha wanazozipata katika kazi zao vizuri ili ziwasaidie wanapostaafu na wanapozeeka na kuwataka wajiunge  na SHIWATA ili wapate nyumba za gharama nafuu katika kijiji chao cha Mwanzega, Mkuranga.

mwisho

No comments:

Post a Comment

Advertising Here